Africa Environment Day

Posted on: March 3rd, 2017

Halmashauri ya Manispaa ya Musoma yaadhimisha siku ya Mazingira Afrika kwa kupanda miti 7,695.

 

Mkuu wa Wilaya ya Musoma Mhe. Dr. Vincent Anney Naano ameongoza zoezi la upandaji miti 7695 katika maadhimisho ya siku ya mazingira Afrika yaliyofanyika katika shule ya sekondari Kiara.

Akihutubia umma wa wanafunzi na wananchi waliojitokeza katika maadhimisho hayo, mkuu wa wilaya aliwataka watu wote kujihusisha na utunzaji wa mazingira kwa kuwa mazingira yana uhusiano mkubwa na ustawi wa binadamu.

“Maendeleo yanayohitajika Duniani kote leo hususan nchi yetu ni Maendeleo endelevu(sustainable development) ambayo maana yake ni maendeleo yanayomwezesha binadamu wa kizazi cha leo kupata mahitaji yake, bila kuathiri uwezekano wa vizazi vijavyo kupata mahitaji yao”.Alisema

Aidha, Dr. Naano aliongeza kuwa “kamwe hatuwezi kufikia maendeleo endelevu bila kutunza mazingira yetu.Hii ina maana kuwa, mazingira ndicho kikapu kinachohifadhi mahitaji yote ya binadamu”

Dr. Naano alitoa wito kwa wananchi wote wa halmashauri ya manispaa ya Musoma kuitikia kwa moyo mmoja zoezi la upandaji miti kwa kila kaya kupande miti isiyopungua mitatu (3) na kuisimamia hadi ikue.

Wakati huo huo Dr. Naano amewataka wanafunzi kujituma katika masomo yao na kuepukana na vitendo vitakavyoathiri maendeleo yao kitaaluma.

Akionekana kurofurahishwa na matokeo ya kidato cha nne kwa mwaka 2016 katika shule ya Kiara mkuu wa Wilaya alisema “Haiwezekani kati ya wanafunzi zaidi ya 200 waliofanya mitihani, mwanafunzi mmoja tu ndiye aliyepata daraja la kwanza kuna kubwa ya kufanya”. 

Kwa upande mwingine Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma Fidelica G. Myovella amesisitiza suala la utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti na kuitunza kwa maendeleo endelevu.

Maadhimisho ya siku ya mazingira Afrika hufanyika kila mwaka tarehe 03. Machi