Baraza la Madiwani latunga Sheria Ndogo Mpya

Posted on: August 3rd, 2017

Baraza la Madiwani latunga jumla ya Sheria Ndogo Tisa.

Kikao cha baraza la madiwani kilichoketi tarehe 02.08.2017 kimejadili na kupitisha jumla ya sheria ndogo tisa ambazo zimefanyiwa marekebisho na nyingine kutungwa upya.

Sheria ambazo zimefanyiwa marekebisho ni pamoja na ushuru wa huduma, usimamizi wa masoko,magulio na minada,ada ya uzoaji, utupaji taka na usafi wa mazingira pamoja na ada na ushuru mbalimbali.

Aidha, sheria ndogo zinazopendekezwa ni pamoja na ada ya uthibiti na uchimbaji madini ya ujenzi, Uthibiti na usimamizi rasilimali za uvuvi katika mialo, Ulinzi wa Umma pamoja na Kilimo na usalama wa chakula.

Mapendekezo ya utunzi wa sharia mpya na marekebisho yake yanatokana na ukweli kwamba sheria zilizopo sasa ni za muda mrefu na haziendani na uhalisia wa sasa.Mara ya mwisho baraza la madiwani kutunga sheria ndogo ilikuwa mwaka 2010.

Awali akiwasilisha rasimu ya sheria mpya mwanasheria wa Manispaa Bi. Savella Paulo kwa niaba ya Mkurugenzi aliueleza mkutano wa Baraza kuwa sheria zinazopendekezwa zimepitia taratibu zote kabla ya kuletwa katika kikao cha baraza.

Sheria hizo zinalenga kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri na kuongeza uwezo wa Halmashauri kujitegemea pamoja na kuweka mazingira bora ya utoaji huduma kwa umma.

Akihitimisha hoja ya kujadili na kupitisha sheria hizo ndogo Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa Mhe. William Gumbo aliueleza mkutano wa baraza kuwa mchakato wa kutunga sheria ndogo ukikamilika utatoa nafuu kubwa katika ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri.

“Sheria hizi ni muhimu sana kwa ajili ya kuongeza wigo wa mapato yetu ikizingatiwa kuwa Halmashauri ina upungufu mkubwa wa vyanzo vya mapato ambao unapelekea ukusanyaji wa mapato kuwa finyu na usiokidhi mahitaji ya Halmashauri katika utoaji huduma” alisema Mhe. Gumbo.

Jitihada za kutunga na kuboresha sheria ndogo zinakuja wakati serikali kuu ikiwa tayari imeondoa baadhi ya vyanzo vilivyokuwa vinakusanywa na halmashauri kama kodi ya majengo, kodi ya mabango, pamoja na kodi ya hotel.

Sheria hizi zinatarajiwa kupekekwa katika wizara ya Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa ajili ya kuidhinishwa tayari kwa kutumika kama sheria rasmi.