Halmashauri ya Manispaa ya Musoma yajibu jumla Hoja 61

Posted on: July 25th, 2017

Halmashauri ya Manispaa ya Musoma yajibu jumla ya Hoja 61.

Kamati ya Fedha na Uongozi imeridhia majibu ya hoja 61 za ukaguzi yaliyojibiwa na timu ya wataalamu katika kikao chake kilichofanyika tarehe 25.07.2017 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri.

Majibu ya hoja hizo 61 yanahusu hoja za mwaka 2015/2016 ambapo katika mwaka huo Halmashauri ya Manispaa ya Musoma ilipata hati safi.

Akiongea katika kikao hicho Mstahiki Meya Mhe.William Gumbo aliipongeza ofisi ya Mkurugenzi kwa utendaji kazi uliotukuka na ushirikiano utekelezaji wa shughuli za Serikali.

“Hati safi iliyopatikana inatokana na ari kubwa ya uwajibikaji katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya serikali pamoja na ushirikiano miongoni mwa watumishi” alisema.

Mhe. Gumbo aliongeza kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanya ili kuhakikisha kuwa hoja za ukaguzi zinapungua hata ikiwezekana kufutika kabisa.

“Hoja hizi za ukaguzi zinaletwa na watumishi na ni watumishi hao hao wanaoweza kuzuia hoja hizo zisitokee kwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu” Alisema.

Aidha, aliongeza kuwa “Ikiwa watumishi wataongeza kasi ya utendaji kazi kwa kiwango cha juu ufanisi utaongezeka kwa kuondokana na hoja za ukaguzi”.

Upatikanaji wa hati safi ya ukaguzi unaiweka halmashauri ya Manispaa ya Musoma katika nafasi nzuri na kuifanya kuwa miongoni mwa Halmashauri nchini zitazotekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria,kanuni na taratibu.