Makamu wa Rais Atembelea Manispaa ya Musoma

Posted on: June 8th, 2017

Samia Afananisha vita ya Uvuvi Haramu na Madawa ya Kulevya

Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu ameziagiza kamati zote za ulinzi na usalama Mkoa wa Mara kuhakikisha suala la uvuvi haramu linakwisha katika mkoa wa mara.

Makamu wa Rais aliyasema hayo katika ziara yake aliyoifanya katika Wilaya ya Musoma ambapo alitembelea miradi ya ujenzi wa hospitali ya rufaa ya Mkoa, ujenzi wa barabara za lami KM 9.867, kiwanda cha uchakataji wa samaki na mradi wa maji.

Akihutubia Mamia ya wananchi katika uwanja wa Mukendo makamu wa Rais aliwataka wananchi kushikamana katika utunzaji wa mazingira ikiwa ni pamoja na kupiga vita uvuvi haramu.

“Vita dhidi ya uvuvi haramu ni sawa na vita dhidi ya dawa za kulevya. Naziagiza kamati za ulinzi na usalama za Mikoa na Wilaya kuhakikisha uvuvi haramu unakomeshwa” alisema.

Aliongeza kuwa “ Katika mapambano ya uvuvi haramu ni muhimu kutumia kila silaha kuhakikisha hali hii haiendelei na kuathiri azma ya serikali kuhakikisha kunakuwa na uvuvi endelevu inafikiwa.

Mhe. Samia aliwakumbusha wananchi kuwa viwanda vingi vya samaki havifanyi kazi kutokana na samaki kutokidhi mahitaji ya viwanda hivyo hali inayosababishwa na uvuvi haramu.

“Kati ya  viwanda vinne vilivyopo katika Manispaa ya Musoma ni kiwanda kimoja tu ndicho kinafanya kazi na viwanda vingine vilivyosalia vimefungwa kutokana na kutokuwapo kwa samaki wa kutosha kuhudumia viwanda vyote” Alisema.

Akemea Mimba za Utotoni

Kuhusu suala la mimba za utotoni makamu wa Rais aliwaonya watu wenye tabia za kuwapa uja uzito watoto wa shule kuwa serikali ipo makini na kila atakayebainika atachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwa ni pamoja na kufungwa jela miaka 30.

Aliwataka pia wazazi kuwa wakali na kutoshirikiana na watu wanaokatisha ndoto za watoto wa kike kwa kuwapa ujauzito.

“Kuanzia sasa serikali haitakuwa na salia mtume kwa majangiri yanayokatisha ndoto za watoto wa kike na kila mazazi atakaeshirikiana na mtu aliyempa mwanafunzi mimba wote watachukuliwa hatua kali” alisema.

Aidha, akizungumza kuhusu suala la uhaba wa chakula Mhe. Samia alisema serikali kamwe haitaleta chakula kwa wananchi wavivu na kuwataka wananchi kufanya kazi kwa bidii ili kujipatia chakula.

“Chakula kitaletwa kwa wananchi wenye jitihada na kitauzwa kwa bei nafuu “ alisema.

Makamu wa Rais yupo Mkoani Mara kwa ziara ya siku tano ambapo katika ziara hiyo anakusudiwa kutembelea, kuzindua na kufungua miradi mbalimbali ya maendeleo.