Miradi yenye thamani ya Bilioni 1.1 yazinduliwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru

Posted on: August 28th, 2017

Miradi yenye thamani ya Bilioni 1.1 yazinduliwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru

Mwenge wa Uhuru umefungua,kuzindua na kuweka mawe ya msingi katika jumla ya miradi 7 ya maendeleo iliyogharimu jumla ya shilingi bilioni 1.1 katika Halmashauri ya Manispaa ya Musoma.

Ziara ya Mwenge wa Uhuru 2017 ilifanyika katika Halmashauri ya Manispaa ya Musoma tarehe 27.08.2017 ukutokea katika Halmashauri ya Wilaya ya Butiama.

Miradi ya maendeleo iliyotembelewa, kuzinduliwa, kufunguliwa na kuwekewa mawe ya msingi ilikuwa ni pamoja na ufunguzi wa wodi ya wazazi, Ufunguzi wa vyumba 4 vya madarasa katika shule ya msingi Mwisenge, Ufunguzi wa vyumba 4 vya madarasa na klabu ya Mazingira shule ya sekondari Nyasho.

Miradi mingine iliyotembelewa na kufunguliwa ni pamoja na Ufunguzi wa kiwanda cha kuzalisha maji ya Kunywa, Uzinduzi wa kituo cha damu salama, Kutembelea mradi wa ufugaji wa samaki pamoja na ufunguzi wa barabara ya FFU-Nyasho Cabin M 330.

Awali akisoma risala ya utii kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mkuu wa  Wilaya ya Musoma Dr. Vicent Naano alimweleza kiongozi wa mbio za Mwenge kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma imekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza kauli mbiu ya Serikali ya viwanda kwa vitendo ambapo maeneo ya uwekezaji wa viwanda yametengwa ikiwa pamoja na kuanza ujenzi wa viwanda hivyo.

“Naomba nikuhakikishie kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma iko makini katika kutekeleza maagizo yote na sera zinazoelekeza katika uwajibikaji na ujenzi wa uchumi madhubuti wa wananchi wa Manispaa ya Musoma” alisema.

Dr. Vicent aliongeza kuwa katika kuongeza wigo wa ajira za vijana Manispaa ya musoma imetenga maeneo maalum kwa ajili ya biashara za vijana na akina mama katika eneo la SIDO lililopo kata ya Nyakato.

Akitoa ujumbe wa Mwenge kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru 2017 Amour Hamad Amour aliitaka Halmashauri ya Manispaa ya Musoma kuhakikisha inaweka mazingira Mazuri ya Biashara ili kuongeza mapato yake.

“Ni vyema sasa mkaanza kufikiri namna nzuri ya kuwawezesha machinga kufanya biashara zao vizuri ikiwa ni pamoja na kuwaboreshea mazingira ya kufanyika shughuli zao ili walipe kodi na serikali iongeze mapato” alisema.

Ndugu Amour alisisitiza kauli mbiu ya ujenzi wa viwanda pamoja na umuhimu wa kuongeza thamani katika bidhaa zinazozalishwa na wajasiliamali wadogo.

“Niwaombe sana wafanya biashara wote muda wa kuuza malighafi umepitwa na wakati na badala yake ni vyema sasa wafanya biashara wetu wakaanza kufikiria kuuza bidhaa zilizoongezwa thamani” alisisitiza.

Aidha, ndugu Amour aliwataka wadau wote wa maendeleo pamoja na wananchi kupiga vita rushwa, Malaria, dawa za kulevya pamoja na mimba za utotoni ambazo zimekuwa kikwazo kikubwa kwa watoto wengi wa kike katika kuendelea na masomo yao.

Mwenge wa Uhuru hukimbizwa kila mwaka nchi nzima lengo kubwa likiwa kuhamasisha jitihada zinazofanywa na serikali katika kuleta maendeleo na ustawi wa jamii pamoja na kujenga uzalendo miongoni mwa watanzania.