Musoma Municipal Council gets its Master Plan

Posted on: April 27th, 2017

Manispaa ya Musoma yazaliwa upya

Mpango kabambe wa matumizi bora ya ardhi wa Manispaa ya Musoma umezinduliwa rasmi leo na Mhe. William Lukuvi, waziri wa ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi tukio lililofanyika makao Makao ya Manispaa ya Musoma.

Mpango huo utakuwa  wa miaka 20, ambapo utatekelezwa kuanzia mwaka 2015-2035 ukienda sambamba na uendelezaji wa miundo mbinu ya Manispaa ya Musoma.

Akihutubia kabla ya uzinduzi wa mpango huo, waziri Lukuzi ameitaka Halmashauri kuandaa mpango mkakati wa utekelezaji wa mpango wa matumizi bora ya ardhi.

Ameongeza kuwa halmashauri inahitaji kuutafsiri mpango huo ili ueleweke vizuri kwa wananchi wote hali itakayosaidia utekelezaji wa mpango huo kwa rahisi na rafiki.

Aidha, mhe. Lukuvi amesema kuwa kamati ya mipango miji na mazingira inalo jukumu kubwa kuhakikisha mpango kabambe wa matumizi bora ya ardhi unasimamiwa vizuri.

 

“Hatua inayofuata baada ya kupatikana mpango kabambe wa   matumizi bora ya ardhi shabaha ya pili ni kuutengenezea mpango kina ili kufikia malengo yaliyokusudiwa” alisema.

Hata hivyo, Mhe. Lukuvi amepiga marufuku ujenzi wowote bila kuwa na kibali cha ujenzi, ambapo ametoa rai kwa Halmashauri kuondoa urasimu katika utoaji wa vibali vya ujenzi.

“Mtu akijenga bila kibali cha ujenzi nyumba hiyo ibomolewe mara

 Moja. Lazima kuwe na masharti ya uendelezaji mji” alisema.

Aliongeza kuwa “ Lengo kuu la upatikanaji wa mpango huu pamoja na uboreshaji miundombinu ni kuongeza wigo kwa serikali kukusanya kodi”.

Mhe. Lukuvi amesisitiza kuwa Halmashauri inalo jukumu kubwa katika kuhakikisha kodi zitokanazo na ardhi zinalipwa kwa wakati na wamiliki wote wa ardhi.

Mhe. Lukuvi pia ameikumbusha halmashauri ya Manispaa ya Musoma kuongeza kasi katika zoezi la urasimishaji wa makazi holela ili makazi hayo yawe rasmi na kuwasaidia wananchi katika upatikanaji wa huduma mbalimbali zikiwamo huduma za kibenki.

Zoezi la utengenezaji wa mpango kabambe wa matumizi bora ya ardhi lilianza mwaka 2013, na kukamilika mwaka 2017 kwa ajili ya maendelezo yanayohitajika katika Manispaa ya Musoma.