Ukaribisho

Neno la Mtahiki Meya

Tangu kuasisiwa kwake Halmashauri ya Manispaa ya Musoma imekuwa katika jitihada za makusudi katika kuwaletea wananchi wake maendeleo katika nyanja zote ikiwamo uchumi, kijamii, kitamaduni, kisiasa na uboreshaji miundombinu unaoendana na mabadiliko ya haraka katika jamii. Kwa kawaida mchakato wa maendeleo ni endelevu, hivyo Halmashauri ya manispaa ya Musoma imekuwa ikitumia rasilimali zake zote kuhakikisha azma hii inatimilika.

Katika kipindi chote hiki Halimashauri imeshuhudia mageuzi makubwa ya kiutendaji kitaifa na kimataifa. Hali hii inatoa tafsiri pana kuwa nyakati zimebadilika sana. Katika dhana hii serikali imekuwa ikitekeleza programu mbalimbali ili kuendana na wakati na mabadiliko ya mfumo wa kiutendaji yanayotokea duniani kote.

Serikali imekuwa katika utekelezaji wa programu ya maboresho katikati ya Miaka ya 90 pamoja na programu nyingine nyingi zilizofuata ili kuongeza ufanisi na tija katika kuwaletea wananchi maendeleo. Aidha, mwaka 2011 serikali ilisaini mkataba wa kimataifa wa makuballiano ya kuongeza uwazi serikalini (Open Government Partnership) Mkataba uliolenga kuongeza ushirikishaji wa wananchi katika maendeleo yao.

Ukamilishaji wa tovuti hii ni moja ya nyenzo muhimu katika kuongeza ushirikishaji wa wananchi na kuongeza uelewa wao katika masuala mbalimbali yanayotekelezwa na Halmashauri yao. Imani yangu ni kuwa wananchi wataitumia fursa hii muhimu kwa ajili ya maendeleo yao kwa kupata taarifa mbalimbali ambazo zitawasaidia kuboresha shughuli zao mbalimbali.

Tunaomba ushirikiano wenu katika katika utoaji wa maoni juu ya namna bora ya kuboresha huduma zetu pamoja na kupata taarifa zinazowahusu. Natoa wito kwa viongozi mbalimbali na watumishi kuwa mstari wa mbele katika kutoa taarifa muhimu kupitia tovuti hii. 

Mwisho tunatarajia kupata ushirikiano mzuri kwa wadau wote katika upashanaji wa taarifa mbalimbali ambao unalenga kuleta mafanikio katika manispaa yetu ya Musoma.

Ahsanteni